News
Watumishi wa Wizara ya Nishati Wahimizwa Kupendana na Kushirikiana Kazini.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe, Dkt. Doto Biteko amewahamasisha Watumishi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kutoa huduma bora kwa wananchi huku akisema Wizara anayoisimamia ni ya kutenda sana na kusema kidogo.
Amesema hayo leo tarehe 27 Julai 2024, wakati wa Bonanza la Nishati aliloliandaa kwa Watumishi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake ambalo limefanyika Jijini Dodoma likibebwa na Kaulimbiu Shiriki Michezo Imarisha Afya.
Mhe.Dkt.Biteko amesema, “Sekta ya Nishati ni muhimu kwenye ujenzi wa uchumi wa nchi yetu na kwamba Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatutegemea sisi ili kuweza kutoa huduma hii muhimu kwa wananchi, hivyo watumishi tupendane, tushirikiane na kufanya kazi kwa bidi zaidi ili kusukuma mbele gurudumu la Nishati.
Kuhusu Bonanza hilo la Nishati, Mhe.Dkt. Biteko ameeleza kufurahishwa kwake na morali waliyokuwa nayo Watumishi ambao wameshiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali na kuahidi kuwa huo utakuwa ni utaratibu wa kila mwaka mara baada ya kufanyika kwa Bunge la Bajeti.
Ameongeza kuwa, nia ya kufanya Bonanza la Watumishi ni kuhamasishana ili kuweza kutoa huduma bora zaidi kwa watanzania kwa sababu wanaitegemea Wizara ya Nishati na Taasisi zake katika kupata huduma hiyo.
Aidha, amewapongeza Watumishi walioshinda michezo mbalimbali katika bonanza hilo wakiwemo kutoka Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi TGDC baada ya kuzawadiwa medali mbalimbali zilizotolewa kwa watumishi walioshinda michezo hiyo.
Mhe.Dkt.Biteko alimaliza kwa kuwapongeza viongozi walioshirikiana katika kuhakikisha bonanza hili linafanikiwa.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu , Mhe. Jenista Mhagama ameeleza kufurahishwa na jinsi Bonanza la Nishati lilivyofanikiwa na kusema kuwa huo ni muitikio wa nia ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa na afya njema na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo dawa yake kubwa ni mazoezi.
Amesema kuwa, michezo inaimarisha afya inajenga umoja, inaleta furaha na kujenga maarifa mapya ya kuwatumikia watanzania hivyo amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko kwa kuasisi Bonanza hilo muhimu kwa Watumishi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amemshukuru Dkt. Biteko kwa kuanzisha Bonanza hilo ambalo amesema linadumisha upendo miongoni mwa Watumishi, umoja, kuwawezesha wafanyakazi kufahamiana zaidi na kuwaimarisha Watumishi.
Amesema kuwa, anaamini Watumishi wamepata motisha ya kazi kupitia bonanza hilo pamoja na hamasa ya kujipanga na kujiimarisha kwa ajili ya michezo inayofuata.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe.Rosemary Senyamule, ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kufanya Bonanza hilo mkoani Dodoma hali ambayo imezidi kulifaharisha Jiji la Dodoma na kuchagiza uchumi na kuahidi kuwa, Serikali mkoani Dodoma itaendelea kuwahamasisha wananchi kufanya mazoezi kama ambavyo Viongozi Wakuu wa Nchi wanahimiza ili kuimarisha afya.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amemshukuru Dkt. Biteko kwa wazo lake la Bonanza ambalo limeleta hamasa kubwa kwa watumishi na kuahidi kwamba Bonanza hilo sasa litafanyika kila mwaka baada ya kupinduka mwaka wa fedha.
Amesema Taasisi zote chini ya Wizara Nishati zimeshirki bonanza hilo ikiwemo Kampuni Tanzu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dkt. James Andilile amemshukuru Dkt. Biteko kwa kuthamini afya za Watumishi, na kueleza kuwa, limewawezesha Wakuu wa Taasisi kujadiliana masuala mbalimbali na kupata majawabu ya baadhi ya masuala.
Kwa nyakati tofauti, Watumishi wa Wizara na Taasisi walioshiriki Bonanza la Nishati wamemshukuru Dkt. Biteko kwa kuanzisha bonanza hilo ambalo wamesema kuwa si tu limechangia kuimarisha afya zao bali pia limewawezesha kufahamiana na watumishi wengine ndani ya Sekta ya Nishati.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ametunukiwa nishani ya michezo ikiwa ni kutambua mchango wake katika ufanikishaji wa Bonanza la Nishati huku wazo la kuanzishwa kwa bonanza hilo likianzia kwake.
Baadhi ya Michezo iliyofanyika kwenye Bonanza hilo ni Kupokezana vijiti wanaume, Kupokezana Vijiti Wanawake, Rede, Karata, Riadha, Kukimbia na yai, Kukimbia ndani ya gunia, Kukimbia na maji kwenye glasi, Kupenya ndani ya pipa, Mpira wa miguu, Mpira wa Pete, Bao na Karata n.k ambapo Shirika la Umeme Tanzania pamoja na watumishi wa TGDC walipata zawadi za Medali, kuku pamoja na kikombe.