News

Posted date: 14-Jan-2025

Washiriki wa Kozi ya NDC toka Chuo cha Taifa cha Ulinzi - Tanzania wafanya Ziara ya Mafunzo Katika Mradi wa Jotoardhi wa Songwe

News Images

Katika kukamilisha sehemu ya mafunzo yake kwa wanazuoni, Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kimefanya ziara ya mafunzo kwa vitendo kwa washiriki wake kupitia Mradi wa Jotoardhi Songwe unaendelezwa na Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) Januari 13, 2025.

Ziara hiyo ni sehemu ya muendelezo wa mafunzo ya Usalama na Stratejia inayohusisha Maafisa Wakuu wa Jeshi toka Mataifa mbalimbali, Maafisa Wakuu toka Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Watumishi wa Sekta za Umma ikilenga kuimarisha ushirikiano wa Kikanda na kuboresha mbinu za Kiulinzi kupitia teknolojia na ujuzi endelevu

Washiriki hao ambao ni Maafisa Wakuu wa Jeshi toka nchi za Tanzania, Bangladesh, Burundi, Kenya, Namibia na Uganda, Maafisa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Watumishi wa Sekta za Umma walitembelea mradi wa Jotoardhi wa Songwe kwa lengo kuboresha uelewa wao kuhusu nishati ya Jotoardhi ambao walifurahishwa na kustaajabishwa kwa jinsi Tanzania ilivyobarikiwa na rasilimali za kutosha ikiwemo ya jotoardhi.

Ziara hiyo iliongozwa na Brigedia Jenerali Method Kamugisha Matunda ambaye ni Mkufunzi Mwandamizi Elekezi wa Jeshi la Nchi Kavu ambaye alionyesha furaha yake kwa kushuhudia hatua za maendeleo zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi inayotokana na Jotoardhi.

Akiongea baada ya timu anayoiongoza kupata maelezo na kupitishwa kwenye maeneo tofauti Brigedia Jenerali Matunda alisema, "Nishati ni moja ya sekta nyeti inayochangia kuimarisha Usalama wa Taifa, hivyo Jotoardhi itakuwa mkombozi na chanzo cha uhakika cha nishati safi na kuimarisha Usalama nchini." Aliongeza kuwa nishati safi kama Jotoardhi ina nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya nchi Kiusalama na Kiuchumi, huku akiahidi kurejea tena kutembelea mradi huo na kushuhudia maendeleo zaidi.

Mradi wa Jotoardhi wa Songwe unaendelezwa na kusimamiwa na Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) wenye lengo la kukuza upatikanaji wa nishati mbadala nchini. Mradi huu una umuhimu mkubwa si tu kwa sekta ya ulinzi, bali pia kwa uchumi wa taifa na kulinda mazingira kwa kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati visivyo endelevu..

Kwa upande wake Bw. Albano Mahecha ambaye ni Meneja huduma za Jiosayansi akimwakilisha Meneja Mkuu TGDC alielezea hatua iliyofikiwa katika uendelezaji wa jotoardhi Tanzania, ikiwemo hatua za utafiti kuelekea uzalishaji umeme unaotokana na Jotoardhi ambapo TGDC itaanza na mradi wa Ngozi, Kiejo-Mbaka na kisha kuendelea na Songwe. Awamu ya kwanza kuelekea uzalishaji umeme inahusisha uchorongaji wa visima vya uhakiki mradi wa Megawati 30 katika Mradi wa Ngozi.

Aidha Mjiolojia Mahecha alielezea fursa zilizopo katika rasilimali za Jotoardhi ikiwemo uzalishaji umeme na matumizi ya moja kwa moja ya Nishati hiyo katika kilimo na ufugaji kama ambavyo mradi wa Songwe umeonesha kupitia miradi ya mifano inayoendelezwa eneo la Songwe Majimoto.

Mwisho, Mjilojia Mahecha aliwashukuru NDC kwa kutembelea mradi wa Songwe na kuonyesha umuhimu wa mradi huu katika usalama wa nchi katika Maeneo ya nishati na chakula kupitia kilimo.