News

Posted date: 22-Feb-2022

Umeme jotoardhi utayaweka mazingira salama

News Images

Na Mwandishi wetu

MOJA ya kichocheo cha maendeleo duniani ni uwepo wa nishati ya uhakika, salama na bora ambayo itaweza kuchangia uzalishaji wa bidhaa kwa gharama nafuu na kutunza mazingira.

Katika nchi zilizoendelea juhudi za uzalishaji wa nishati zimejikita kwenye nishati jadidifu ambapo msingi mkubwa umejikita kwenye usalama, uhakika unafuu na uendelevu.

Wataalam wa uchumi wanasema ukosefu wa nishati ya uhakika unapelekea bidhaa zinazozalishwa viwandani kuuzwa bei kubwa.

Lakini pia gharama kubwa ya nishati ya umeme katika nchi za Afrika inatajwa kuwa ni sababu kubwa ya kuuza malighafi kuliko bidhaa.

Tanzania ni moja ya nchi ambayo Desemba 9, mwaka huu inaadhimisha miaka 60 ya uhuru, lakini bado uhakika wa nishati ambayo inaweza kutumika katika kuchakata malighafi viwandani na bidhaa ni asilimia kidogo.

Kwa taarifa za sasa gridi ya taifa ina megawati 1,605 ambapo umeme wa gesi asili ni megawati 900 sawa na asilimia 64.1, maji megawati 508 asilimia 31.8 nishati jadidifu megawati 58 asilimia 025 na mafuta megawati 139 asilimia 3.7.

Kiwango hicho cha megawati 1,605 kinasemekana kinakidhi mahitaji ya Watanzania ila kwa upande wa mazingira kinachangia uharibifu.

Katika kuhakikisha kuwa nishati ya umeme inapatikana kwa uhakika Serikali ina mipango na mikakati mbalimbali ambayo ni kuhakikisha ifikapo 2025 Tanzania iwe na megawati 1,100 za nishati jadidifu.

Maeneo ambayo yanatarajiwa kupewa kipaumbele cha kuzalisha nishati jadidifu ni umeme jua, upepo na jotoardhi.

Nchi kama Kenya, Ethiopia, Iceland na Marekani zimepiga hatua katika uvunaji na utumiaji wa nishati jadidifu hasa jotoardhi (Geothermal Energy).

Marekani ina nishati jadidifu asilimia 12, makaa ya mawe asilimia 10, nyukilia asilimia 9, mafuta asilimia 35 na gesi asilia 34.

Tanzania imejaliwa Bonde la Ufa ambapo tafiti zimeonesha kuna nishati jadidifu itokanayo na jotoardhi ipo nyingi.

Tafiti nyingi zimefanywa na zimethibitisha kuwa aina hii ya nishati ni ya uhakika, safi, haichafui mazingira na ni endelevu.

Nishati ya jotoardhi inatokana na joto asilia linalozalishwa katikati ya ganda na kiini, kitovu cha dunia na usafiri kwa njia ya mpitisho ama msafara na kuhifadhiwa ndani ya ganda la dunia.

Kupitia fursa hii, Tanzania imeunda Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), ikiwa ni Kampuni Tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Uanzishwaji wa TGDC ni kuhakikisha umeme wa kutosha unapatikana kupitia na kuingia kwenye gridi ya taifa hivyo kupunguza gharama za nishati hiyo.

Mhandisi Cynthia Kuringe kutoka TGDC, anasema dira ya TGDC ni kuwa kampuni ya maendeleo ya jotoardhi inayoongoza na yenye ushindani katika Ukanda wa Afrika Mashariki na kuhudumia kizazi cha sasa na kijacho kwa nishati ya uhakika, yenye gharama nafuu na rafiki na mazingira.

“Dhamira yetu ni kutoa huduma za maendeleo ya nishati ya jotoardhi za uhakika na ufanisi, kusaidia dira ya taifa ya maendeleo ya taifa, kuongeza ajira mpya

Kuringe anasema nishati ya jotoardhi ni endelevu, rafiki wa mazingira, haitegemei hali ya hewa na ina matumizi mengine tofauti na umeme.

Anasema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi ya jotoardhi ambapo uwekezaji ukiwepo kuna zaidi ya megawati 5,000 za nishati hiyo ambayo ni jadidifu.

“Tanzania imejaliwa kuwa na nishati jadidifu ya joto ardhi ambapo utafiti unaonesha kuna uwezekano wa kupata megawati 5,000 katika maeneo 52 ya mikoa 16,” anasema.

Mhandisi Kuringe anataja mikoa yenye jotoardhi ni Arusha, Dodoma, Iringa, Morogoro, Mbeya, Kilimanjaro, Kagera, Katavi, Shinyanga, Songwe, Manyara, Rukwa, Singida na Tanga.

Anasema katika Mkoa wa Arusha nishati jadidifu ya jotoardhi inapatikana Meru, Eyasi, Natroni na Ngorongoro, Dodoma inapatika Gonga, Mpondi, Takwa na Kondoa na Iringa ni eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

“Mkoa wa Kagera ni Mtagara, Katavi ni Maji Moto na Mpimbwe, Kilimanjaro ni Rundugai na Nyumba ya Mungu, Manyara ni Majimoto, Balangidalalu, Kiria, Manyegehi na Balangida,” anasema.

Kuringe anasema Mkoa wa Mara nishati ya jotoardhi inapatikana eneo la Maji Moto, Mbeya ni Kalambo, Mahembe, Mampula, Kasumulo, Udindilwa, Ngozi na Morogoro ni Kisaki, Mtende na Tagalala.

Aidha, anasema Mkoa wa Pwani utafiti unaonesha kuwa jotoardhi ipo eneo la Luhoi na Utete, Rukwa ni Kanazi na Mapu, Shinyanga ni Ibadakuli, Singida ni Msule, Hika na Isanja, Songwe ni Maji Moto na Ivuna na Tanga ni Bombo, Amboni na Kidugalo.

Kuringe anasema katika kufanikisha zoezi zima hatua tatu muhimu zifanyine ambazo ni utafiti, uhakiki wa rasilimali na uendelezaji na uzalishaji.

Anasema katika hatua ya utafiti kuna hatua ya utafiti wa awali, wakina juu ya ardhi (jiolojia, jiofizikia na jiokemia). “Uhakiki wa rasilimali utajikita kwenye thathmini ya kimazingira, uchorongaji wa visima vya uhakiki na upembuzi yakinifu wa awali,” anasema.

Mhandisi huyo wa TGDC anasema kwenye uendelezaji na uzalishaji zipo hatua mbalimbali kama uchorongaji visima vya uzalishaji, ujenzi wa mitambo, uzalishaji, uendeshaji na uangalizi.

Anasema utafiti unaonesha kuwa nchi 90 duniani zina maenero yenye rasilimali ya jotoardhi ambapo nchi 26 zinazalisha megawati milioni 15.6 za umeme wa jotoardhi ambapo nchi ya Kenya yenyeewe ikizalisha zaidi ya megawati 890.

“Nishati ya jotoardhi sio kwa ajili ya umeme pekee ina matumizi mengine kamae kukausha mazao hivyo ni nishati muhimu kwa kukuza uchumi namaendeleo kwa ujumla,” anasema.

Kuringe anasema shabaha kuu ya TGDC ifikapo mwaka 2025 wawe wamezalisha megawati 200 za umeme wa jotoardhi ambayo itapatikana katika maeneo ya Ngozi, Songwe, Kiejo-Mbaka na Luhoji.

Anasema uchorongaji wa visima vifupi Kiejo-Mbaka, na Ngozi unaendelea na miradi ya majaribio ya matumizi mengine ya jotoardhi inaendelea kutekelezwa katika eneo la Songwe.

Kwa upande wake Mjiolojia John Bosco, anasema nishati jadidifu ina faida nyingi kiuchumi, kijamii, mazingira na maendeleo kutokana na kututumia gharama kubwa ya uwekezaji nan i endelevu.

Anasema pamoja na fursa ya uwepo wa nishati jadidifu nchini kuna changamoto ya kukosekana kwa Sheria na Sera ambayo moja kwa moja inayozungumzia nishati hiyo.

Mtaalam huyo anasema sheria hiyo ipo kijumla hali ambayo inaifanya TANESCO kuwa mzalishaji, msambazaji na mwenye mamlaka hivyo hakuna maamuzi ya kimamlaka katika eneo hilo.

“Leo hii ukienda halmashauri utakuwa ofisa kilimo, elimu, mazingira, maji, afya na nyingine lakini hakuna ofisa nishati ambaye anatakiwa asimamie sheria na sera za sekta hiyo. Kinachooneka sekta hii ipo TANESCO na sio kiwazara katika ngazi hiyo,” anasema.

Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Felschemi Mramba Serikali kupitia Wizara ya Nishati imepanga kutekelezaji maalekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyotoa siku akihutubia Bunge kuwa hadi 2025 wawe wamezalisha megawati 1,100 za nishati jadidifu.

“Tupo kwenye mchakato wa kuzalisha megawati 500 za umeme jua na upepo ifikapo 2023, lakini pia Kampuni yetu ya Jotoardhi inatarajia kuzalisha megawati 200 hivyo tutakuwa na megawati 700 za nishati jadidifu ifikapo 2024 ,” anasema.

Kamishna Mramba anasema kuanzia mwaka 2023 hadi 2025 wanatarajia kuongeza megawati zingine 400 hivyo lengo la kufikia megawati 1,100 litafanikiwa na kuwa na umeme wa uhakika kwa nchi na kwamba katika eneo la jotoardhi wanatarajia kuzalisha megawati 5,000 kwa ujumla.

Mtaalam huyo wa masuala ya umeme anasema sababu ya Serikali kuwekeza megawati chache ni kutokana na uwezo wa gridi ya taifa ambayo inahitaji megawati chache hivyo wataendelea kuwekeza hatua kwa hatua kwa kuboresha gridi.

“Inawezekana tumechelewa kuwekeza katika eneo la nishati jadidifu, lakini niseme wakati huu ndio wakati sahihi kwani gharam za uzalishaji wakati wa nyuma tungeshindwa kwa sababu bei ya umeme huo ilikuwa ghali,” anasema.

Mramba anasema nishati jadidifu kutokana na tafiti mbalimbali ni salama, inatunza mazingira na endelevu hivyo wanaomba wawekezaji kuwekeza katika eneo hilo.

Anasema Serikali imejipanga kutatua changamoto za kisera na sheria ili kuvutia wawekezaji kuwekeza kwenye nishati jadidifu.

Kamishna Mramba anasema umeme unaozalishwa kwa njia nishati jadidifu utauzwa kwa Shrika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Naye Mjumbe wa Bodi wa Shirika la HakiMadini, Amani Mhinda anasema nishati jadidifu utakomboa taifa kwenye sekta zote.

Anasema nishati jadidifu inatumiwa katika kila kona ya nchi hivyo Serikali ikiweka nguvu itanufaika kwani wananchi wanatambua faida yake.

Mwisho