News

Posted date: 07-Jul-2024

Mhe.Dkt.Kikwete Aipa Heko TGDC, Hatua za Utafutaji Nishati ya Jotoardhi

News Images

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) kufuatia hatua iliyofikiwa katika utafutaji wa nishati jadidifu ya jotoardhi.

Pongezi hizo amezitoa Julai 6, 2024 alipotembelea banda la TGDC ndani ya jengo la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakati wa maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara Dar es Salaam Sabasaba na kusema kazi iliyofanywa ni kubwa na hivyo kampuni iendeleze juhudi hizo ili hatimaye Tanzania iupate umeme unaotokana na jotoardhi.

“ninakumbuka wakati nikiwa madarakani nilifika hadi Olkaria nchini Kenya kwa ajili ya jambo hili, hivyo niwapongeze kwa hatua mliyoifikia”, alimaliza mheshimiwa Dkt.Kikwete.

Akitoa maelezo kwaniaba ya Meneja Mkuu wa TGDC, Bi.Khadija Faru alimweleza Mhe.Dkt.Kikwete kuwa, kwa sasa kampuni inaendelea kutekeleza miradi yake mitano ya kipaumbele yenye lengo la kuzalisha megawati 200 na kwamba kwa mradi wa Ngozi (megawati 70), TGDC ipo katika hatua ya uhakiki wa rasilimali ili iweze kuchimba kwa ajili ya kuzalisha umeme utakaotokana na jotoardhi.

TGDC inaendelea kuwakaribisha wananchi na wadau mbalimbali kutembelea banda lake katika viwanja vya maonesho ili kujifunza ni kwa jinsi gani Tanzania inaweza kuzalisha umeme kwa kupitia nishati ya jotoardhi, nishati iliyo jadidifu na ya uhakika iliyo rafiki wa mazingira.