News

Posted date: 07-Aug-2024

Katibu Mkuu Mramba Aitaka TGDC Kuhamasisha Uwekezaji Kilimo cha Mashamba Makubwa

News Images

Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba ameiagiza Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania TGDC kutafuta na kuhamasisha wawekezaji wa mashamba makubwa ili kuwa na kilimo chenye tija kitakachonufaisha wananchi wengi kitakachowezeshwa na rasilimali ya jotoradhi.

Mhandisi Mramba ametoa agizo hilo leo Agosti 6, 2024 alipotembelea banda la TGDC wakati wa maonesho ya kimataifa ya kilimo Nanenane mwaka 2024 yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma na kusema kwa kufanya hivyo rasilimali ya jotoardhi itaweza kuwanufaisha wananchi wengi zaidi na kuifanya kuwa rahisi, isiyo ghali.

Amesema, “niwapongeze TGDC kwa kutoa elimu ya matumizi ya moja kwa moja yatokanayo na rasilimali ya jotoardhi. Hiki mnachokifanya ndiyo jambo sahihi la kuwafikishia wananchi. Lakini pamoja na hilo, mkawahamishe wawekezaji ili waje kuwekeza kwenye mashamba makubwa yatakayotumia rasilimali ya jotoardhi ili kipatikane kilimo chenye tija na kiwanufaishe wananchi wengi zaidi”, amesema Mhandisi Mramba.

Mhandisi Mramba alienda mbele zaidi na kuipongeza TGDC kwa hatua ilizozifikia katika utafutaji wa nishati ya umeme wa jotoardhi akisisitiza ni muhimu kwa Kampuni kuzalisha umeme kama yalivyo matarajio ya serikali.

Awali akitoa maelezo ya Modo ya mfano kuonesha jinsi gani rasilimali ya jotoardhi inaweza kuwanufaisha wakulima na wafugaji mbele ya katibu mkuu nishati, Mjiokemia Mwandamizi Ariph Kimani alisema, TGDC ni Kampuni iliyojizatiti kuendana na malengo ya Serikali kwa kuhakikisha nchi yetu inapata umeme wa uhakika kama lilivyo lengo kuu la Serikali yetu na baada ya hapo kuhakikisha mkulima na mfugaji wananufaika kupitia rasilimali hiyo.

Mjiokemia Kimani alieleza kuwa pamoja na upatikanaji wa umeme, nishati ya jotoardhi inaweza kuwanufaisha wananchi katika uongezaji thamani wa mazao ya mifugo na kilimo, kwani nishati hiyo huweza kusaidia kilimo cha nyumba kitalu, kukausha mazao, kuwezesha uchakataji wa maziwa, utotoleshaji wa vifaranga, ukaushaji wa Ngozi, ufugaji samaki n.k ambavyo vyote hivyo huendana na maonesho ya nanenane mwaka 2024.

TGDC ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inayomilikiwa na Serikali kwa 100% iliyoanzishwa mwaka 2013 na kuanza shughuli zake rasmi mwaka 2014 ikiwa na jukumu la kuendeleza rasilimali ya jotoradhi nchini ambapo kwa sasa inayo miradi mitano ya kipaumbele yenye lengo la kuzalisha megawati 200 kwa awamu ikiwemo mradi wa Ngozi (MW 70), Kiejo - Mbaka (MW60), Songwe (MW5-38), Luhoi (MW5) na Natron (MW60) ambapo kwa sasa TGDC ipo katika hatua ya maandalizi uchorongaji visima vya uhakiki wa rasilimali ya Jotoardhi.

Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania inaungana na Watanzania wote kwa ujumla katika kuhakikisha kauli mbiu ya nanenane kwa mwaka huu isemayo “chagua viongozi bora wa serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi”, kwani katika uchaguzi wa viongozi bora itapelekea miradi yetu nchini kuendelezwa kwa tija na weledi katika kuipeleka nchi yetu katika uchumi bora duniani kama kauli ya Rais wetu ya mara kwa mara kuifungua nchi yetu kiuchumi.