News

Posted date: 07-Jul-2024

Kamishna Luoga Asisitiza TGDC Kutafuta Wawekezaji wa Umeme wa Jotoardhi.

News Images

Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga amesema, ni muhimu kwa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) kuendelea kuweka msukumo na nguvu zaidi ili kufikia azma ya kuzalisha umeme kupitia nishati jadidifu ya jotoardhi.

Ameyasema hayo Julai 5, 2024 alipotembelea banda la Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) wakati wa maonesho ya 48 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Akiongea baada ya kupata maelezo kutoka wataalam wa kampuni hiyo, mhandisi Luoga ameonesha kufurahishwa na jitihada zinazoendelea kufanyika ili kuhakikisha lengo la kuzalisha umeme huo linafikiwa lakini pia utoaji wa elimu unaoendelea kwenye maonesho haya.

“nimefurahi kufika kwenye banda lenu na hongereni sana kwa elimu mnayoitoa lakini wito wangu ni kwamba tuendelee kuongeza juhudi katika kuhakikisha tunazalisha umeme. Ninatambua jitihada mnazoendelea nazo na hivyo ninawatakia kila la heri katika kufanikisha malengo ya wizara na Taifa kwa ujumla. Vilevile nitoe rai, mtumie maonesho haya kutafuta wawekezaji waje kuwekeza kwenye sekta hii ya nishati jadidifu ya jotoardhi” alimaliza mhandisi Luoga.

Naye Bi.Fatumati Mnzava kwaniaba ya Meneja Mkuu wa TGDC amemuahidi kamishna Luoga kuwa, kila wakati, kampuni imekuwa na jitihada mbalimbali ili kuhakikisha inatoa matokeo na kwa kuthibitisha hilo, watumishi wamejiwekea lengo liitwalo , “mtu mmoja, megawati moja” ikimaanisha kwamba kila mmoja yupo tayari kuhakikisha umeme huo unapatikana.

TGDC inaendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kufika katika banda lake ndani ya jengo la TANESCO wakati maonesho ya sabasaba yanaendelea ili kupata elimu juu ya namna gani Tanzania itanufaika na umeme utokanao na jotoardhi pindi utakapozalishwa.