News

Posted date: 22-Feb-2022

Jotoardhi fursa ya kiuchumi iliyojificha

News Images

Na Mwandishi wetu

TANZANIA ni moja ya nchi yenye rasilimali asili nyingi, ambazo zikitumika ipasavyo zinaweza kufanya mapinduzi ya kiuchumi, maendeleo na jamii.

Baadhi ya rasilimali hizo ni madini, misitu, maji, ardhi yenye rutuba, wanyama, hifadhi, vyanzo vya nishati jadidifu na nyingine nyingi.

Mfano katika eneo la maji inadaiwa kuwa Ziwa Tanganyika ambalo ni la pili kwa ukumbwa baada ya Ziwa Baikal lenye ujazo wa kilomita 23,000 huku Tanganyika likiwa na ujazo wa kilomita 18,900.

Kwa upande wa Ziwa Nyasa lina ujazo wa kilomita 8,500 na Victoria ujazo wa kilomita 2,500 likiwa linaingia mara nane kwenye Ziwa Tanganyika.

Aidha, taarifa zinadai kuwa Ziwa Tanganyika lina asilimia 18.9 ya maji yote safi yaliyopo kwenye uso wa dunia, huku Tanzania tukimilili asilimia 46 ya Ziwa Tanganyika.

Kwa maana hiyo inatufanya Tanzania tumiliki asilimia 8.5 ya maji yote safi yaliyopo kwenye uso wa dunia ambapo ukijumlisha na maji ya Nyasa na Victoria inawezekana Tanzania ikawa inamiliki asilimia 11 ya maji yote yaliyopo kwenye uso wa dunia.

Halikadhalika katika upande wa misitu, wanyama na hifadhi inabainishwa kuwa Tanzania imejaliwa rasilimali hizo za kutosha kuliko nchi nyingine duniani hali ambayo inapelekea kuwa nchi hii ndipo kulikuwa na Bustani ya Eden.

Kubwa kuliko ambalo bado linashabihisha Tanzania kuwa nchi yenye neema ni kuwepo kwa rasilimali za nishati ambazo ni endelevu (nishati jadidifu).

Taarifa zinadai kuwa Tanzania kupitia nishati jadidifu ya upepo, jua, jotoardhi, biomasia na nyingine inaweza kuzalisha megawati zaidi ya 20,000 za umeme ambao unaweza kutumia nchini na kuuza nje.

Katika rasilimali hizi ipo moja ambayo inatambulika kwa jina la jotoardhi ambayo inadaiwa inapopatikana inaweza kusababisha kupatikana rasilimali nyingine zaidi ya tano zinazotumika kwa matumizi mengine.

Kutokana na mazingira hayo nadiriki kusema nishati jadidifu ni fursa ya kiuchumi, kijamii, mazingira na maendeleo iliyojificha Tanzania.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Kato Kabaka anathibitisha kuwa nishati jadidifu ya jotoardhi iwapo ikipatikana inaweza kubadilisha maisha ya Watanzania na Tanzania kwa ujumla.

Anasema katika utafutaji nishati ya jotoardhi pia yanapatikana madini, maji mvuke, maji moto, gesi na umeme jambo ambalo linasaidia sekta nyingine kuguswa hivyo mnyororo wa thamani kutokea.

“Miradi hiyo na mingine ikikamilika itaongeza mnyororo wa thamani katika maendeleo ya sekta mbalimbali za kiuchumi kama viwanda, kilimo, ufugaji, madini, afya, utalii, michezo, sayansi na teknolojia, maji safi na ajira. Hii ndio tafsiri kuwa jotoardhi ni fursa iliyojificha,” anasema.

Mhandisi Kabaka anasema rasilimali jotoardhi inapatikana kwenye maeneo 50 tofauti ya mikoa 16 ambayo ni Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida, Dodoma, Songwe, Mbeya, Pwani, Kigoma, Kagera, Morogoro, Njombe Tanga, Mara, Rukwa na Katavi.

Maeneo 50 ambayo yanaweza kuzalisha nishati ya jotoardhi ni Meru, Eyasi, Manyara, Natron, Ngorongoro, Gonga, Mpondi and Takwa, Kondoa, Ruaha National Parks, Mtagata, Maji Moto (Mpimbwe Municipal).

Mengine ni Rundugai, Nyumba ya Mungu, Majimoto, Balangidalalu, Kiria, Manyegehi na Balangida, Maji moto, Kilambo, Mahombe, Mampulo, Kasumulo, Udindilwa, Ngozi Kisaki, Mtende na Tagalala.

Pia, Luhoi na Utete, Kanazi na Mapu, Ibadakuli, Msule, Hika na Isanja, Maji moto (Songwe) na Ivuna, Bombo, Amboni na Kidugalo

Anasema ukubwa wa eneo ambalo fursa ya jotoardhi inapatikana ni zaidi ya nusu ya mikoa ya Tanzania hivyo ni dhahiri uwekezaji ukiwa mkubwa sekta zote alizozijata awali zitanufaika moja kwa moja.

Kabaka anasema jotoardhi iliyopo Tanzania inaweza kuzalisha mrgawati 5,000 za umeme na megawati 15,000 za joto ambalo ndilo litatumika kwenye kilimo, ufugaji, sayansi na teknolojia, afya hali ambayo itachochea ajira kuongeza na uchumi kukuwa kwa kasi.

“Ni vigumu mtu kuelewa maana halisi ya sisi kusema jotoardhi ni fursa ya kiuchumi iliyojificha, ila uhalisia wake upo kwenye maeneo ambayo yatanufaika na megawati 15,000 za joto ambazo zitazalishwa, lakini pia umeme utakuwa wa uhakika hivyo viwanda kuiongeza uzalishaji,” anasema.

Anasema rasilimali hiyo adimu ambayo inapatikana katika maeneo ambayo yamepitiwa na bonde la ufa inaweza kubadilisha maisha ya Mtanzania na Tanzania kwa ujumla kwani inahusisha sekta zote muhimu.

Mhandisi Kabaka anasema katika kuthibitisha hilo wametekeleza mradi wa mfano wa ufugaji wa kuku ambao ni wa kwanza kutelelezwa hapa Tanzania na duniani na kilimo kwa njia ya jotoardhi ambalo limepatikana kwenye miradi inayoendelea na matokeo yake yamekuwa mazuri.

“Waatalam wanasema kupitia nishati ya jotoardhi unapata gesi, madini, maji moto, maji mvuke na nishati ya umeme hivyo hakuna sababu ya kukunja mkono katika eneo hilo ambalo linachangia ukuaji wa uchumi na maendeleo.

Mhandisi Kabaka anasema hakuna sababu ya Tanzania kubakia kwenye dimbwi la umaskini kwani fursa hiyo ikishirikiana na zingine kama maji, misitu, madini, ardhi yenye rutuba vinapaswa kupaisha uchumi wa Tanzania.

Anasema katika kuhakikisha nishati jadidifu ya jotoardhi inakuwa na tija TGDC, imejipanga ifikapo mwaka 2025 iwe imezalisha megawati 200 za nishati jadidifu na megawati 500 za joto, ambazo zitaweza kuingia kwenye gridi ya taifa, kukuza uchumi na kutunza mazingira.

Meneja huyo anasema TGDC inatekeleza miradi ya kuzalisha megawati hizo kama moja ya majukumu yao ila pia wanapata msukumo kutoka Serikalini na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo marajio ni kwamba ifikapo 2025 kuwepo na megawati 1,100 za nishati jadidifu.

Anasema jotoardhi ni umeme unaozalishwa kutumia shinikizo la mvuke pamoja na joto ambalo husukuma na kuzungusha mitambo ya kuzalisha umeme, huku likiwa na sifa kuu ya endelevu.

“Tumeanza mchakato wa utafutaji megawati 200 za nishati jadidifu itokanayo na jotoardhi katika maeneo Ngozi Mbeya megawati 70 ambapo gharama zake ni takribani dola za Marekani milioni 144,” anasema.

Kabaka anasema utekelezaji wa mradi huo ikiwa pamoja na utafiti na uhakiki ulianza mwezi Septemba 2015 na unatarajiwa kukamilika ifikapo 2023 ambapo kwa sasa hatua iliyofika ni uchorongaji wa visima vya uhakiki.

Meneja huo alitaja mradi mwingine ni Songwe ulioanza 2018, ambao utazalisha megawati tano za umeme na matumizi mengine na utagharimu takribani dola milioni 32.

Anataja mradi mwingine ni Kiejo Mbaka ulipopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya ulioanza mwaka 2017, ambao unatarajiwa kutoa megawati 60 ambapo hatua za utafiti wa awali utaweza kuzalisha megawati 10 na utakamilika mwaka 2024 na utagharimu takribani dola za Marekani milioni 75.

Anasema kwa sasa mradi upo katika hatua za uhakiki rasilimali ya jotoardhi kwa kutumia visima vya uhakiki vitakavyochorongwa eneo la mradi.

“Hatua ya kwanza itakuwa ni uchorongaji wa visima vitatu vya utafiti kwa urefu wa mita 300/75 sentigredi kila kimoja ikiwa na lengo la kuongeza taarifa za kisayansi ambazo zitatoa tathmini bora ya kuchoronga visima virefu,” anasema.

Kabaka anasema hatua ya pili itakuwa kuchoronga visima vinne virefu vya mita 1,500 hadi 1,900 vya uhakiki na baada ya kukamilika hatua hiyo mradi utaingia katika hatua ya uendelezaji ikiwa ni pamoja na kuchoronga visima vya uzalishaji.

“Tumedhamiria kushiriki kukuza uchumi wa Tanzania ndio maana tunapambana kuhakikisha 2025 tumepata megawati 200 za nishati jadidifu na megawati 500 za joto,” anasisistiza.

Mhadisi huyo anataja miradi mingine ni Luhoi mkoani Pwani utakazalisha megawati tano, Natron mkoani Arusha megawati 60 ambayo inatarajiwa kukamilika mwaka 2025.

Kwa upande wake Kamishina Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila anasema serikali inaendelea kuzungumza na wadau mbalimbali ili waje kuwekeza katika eneo hilo kwani fursa hiyo ni muhimu kwa nchi na dunia kwa ujumla.

Mhandisi Rwebangila anasema mikakati yao ni kuhakikisha nishati ya umeme inakuwepo ya uhakika na kwamba ziada ambayo imeonekana kwenye jotoardhi kuwa na joto ambalo linafaa kwa kilimo, ufugaji, utalii na vingine ni fursa ambayo itachangia maisha ya Watanzania kubadilika.

"Sisi kama Serikali tupo pamoja na TGDC, kuhakikisha kuwa rasilimali hii ya jotoardhi ambayo tumebarikiwa inawekezwa ili kutumika hasa kukabiliana na changamoto za umeme nchini na kuchechea ukuaji wa uchumi na utunzaji mazingira.

Tutaendelea kuwasiliana na wawekezaji mbalimbali nje na ndani ili waje wawekeze kwenye eneo hilim kwani hii ni fursa iliyojificha kweli,”alisema.

Mhandisi Rwebangila anasema dunia kwa sasa inahamia kwenye nishati jadidifu hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuungana na Serikali kwenye mpango huo uli uweze kufanmikiwa.

Mwisho