News

Posted date: 28-Jun-2025

Energy Nishati Bonanza in Dodoma, TGDC Participated*

News Images

Dodoma, Juni 28, 2025 — Bonanza la Nishati 2025 limefanyika kwa mafanikio makubwa leo katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, likiwakutanisha watumishi kutoka taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Nishati kwa siku ya michezo, afya na mshikamano.

Bonanza hilo limefunguliwa rasmi na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, aliyesisitiza umuhimu wa michezo kazini kama chachu ya afya bora, ushirikiano, na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma. Hafla hiyo pia imehudhuriwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

Katika bonanza hilo, Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) ilionyesha ushiriki wa hali ya juu, ikiwa ni pamoja na kushiriki kwa mara ya kwanza katika mchezo wa mpira wa miguu. TGDC ilicheza mechi ya utangulizi dhidi ya TANESCO ambapo licha ya kushindwa kwa mabao 4–3, timu hiyo ilionyesha ushindani mkubwa na moyo wa kujituma.

Michezo mingine iliyoshirikisha taasisi mbalimbali ni pamoja na kufukuza kuku, bao, drafti, riadha, na rede ambapo wafanyakazi wa TGDC walishiriki kwa ari na hamasa kubwa. TGDC imefanikiwa kunyakua medali kwenye michezo kadhaa kama vile Riadha, Kukimbia kwenye gunia, kukimbia yai na kukimbia kwenye vikwazo, na pia kwenye kukimbiza kuku.

Bonanza hili limeendelea kuimarisha mshikamano baina ya taasisi za sekta ya nishati huku likihamasisha maadili ya kazi, afya ya mwili na akili, na kukuza utamaduni wa kushirikiana nje ya mazingira ya kazi ya kila siku.