Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania

Tanzania Geothermal Development Company

(TGDC)

TGDC na mkakati wa kuendeleza tafiti za jotoardhi Shinyanga Imewekwa: 27th April, 2018

Mwenyekiti wa Bodi ya TGDC, Beatus Segeja ametembelea eneo la Ibadakuli lililoko Manispaa ya Shinyanga ili kufahamu matokeo ya tafiti za awali za nishati ya jotoardhi na mpango wa TGDC wa kufanya tafiti za kina katika eneo hilo.

Akipatiwa maelezo na Meneja Mkuu wa TGDC, Mhandisi, Kato Kabaka amesema tafiti za awali zinaonesha uwepo wa nishati ya jitoardhi inayoweza kutumika kwa matumizi mbali mbali tafiti za kina zikikamilika.

“Tayari tafiti za awali za eneo hili zinaonesha linafaa zaidi kwa matumizi ya moja kwa moja kama utalii, kilimo na ufugaji,” amefafanua Mhandisi, kabaka.

Ameongeza kuwa kiwango cha joto kilichopo hapo kwa sasa kiko chini kuweza kuzalisha umeme, japo tafiti za kina zikifanyika ndizo zitakazo toa jawabu sahihi kama nishati hiyo inaweza kufaa kuzalisha umeme.

“Kwa sasa tutaongeza msukumo wa tafiti katika eneo hili ili kupata taarifa nyingi za kisayansi zitakazo tusaidia katika kufanya maamuzi ya miradi sahihi ambayo kiuchumi inafaa kuwekeza katika eneo hili,” alieleza Mhandisi, kabaka.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TGDC, Beatus Segeja amesema kuwa kuna haja ya TGDC kuongeza nguvu zaidi katika kuhakikisha taarifa za kina za utafiti zanapatikana ili kuwa na uhakika wa aina ya miradi inayofaa kuwekeza katika eneo hilo.

“Iwapo tafiti zikikamilika na kuonyesha uwepo wa jitoardhi mahali hapa, eneo hili ni rahisi kufikika na lina tija kibiashara kwani liko karibu na Manispaa ya Shinyanga, zaidi liko karibu na barabara ya Shinyanga kwenda Mwanza,” alisisitiza, Segeja.

Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi nchini (Tanzania Geothermal Development Company Limited) TGDC ni Kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) iliyoanzishwa kwa lengo kuu la kusimamia, kutafiti, kuvuna na kuendeleza jotoardhi (Geothermal energy) nchini ili kuongeza vyanzo vya nishati ya umeme pamoja na matumizi mengine ya moja kwa moja.