News

Posted date: 19-Aug-2022

TANESCO ILIVYOZINDUA BODI ZA TGDC NA TCPM

News Images

TANESCO ILIVYOZINDUA BODI ZA TGDC NA TCPM

Kampuni tanzu za Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) Zijulikanazo kama TGDC na TCPM Julai, 2022 zimetambulisha bodi zao mpya za uongozi zitakazosaidia kuongeza ufanisi na utelekezaji wa majukumu mbalimbali ya kampuni hizo ili kuongeza tija kwa shirika.

Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Johari Rotana uliopo jijini Dar es salaam ambapo ulihudhuriwa na wajumbe wa bodi za kampuni mama yani TANESCO pamoja na kampuni zake za TGDC na TCPM.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mwenyekiti wa Bodi ya shirika la umeme Tanzania TANESCO, Omari Issa amesema ni matarajio yao kuwa uteuzi wa bodi hizo mbili utaongeza utekelezaji wa haraka wa majukumu ya Shirika tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

"Bodi ndio kiungo kikubwa sana katika kuendesha kampuni. Kampuni yoyote ile watu wanawekeza, wananunua hisa lakini wanaoendesha bodi ndio wanaoendesha kampuni. Miongoni ya majukumu ya bodi ni pamoja na kupanga mipango ya muda mrefu kujua kampuni inakwenda wapi pamoja na kusimamia utekelezaji wa majukumu" amesema Issa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Maharage Chande ameelezea furaha yake kutokana na upatikanaji wa wajumbe wapya wenye uwezo,uzoefu na weledi.

"Tunategemea baada ya muda mfupi kampuni hizi zitaweza kujiendesha kwa ufanisi lakini zitaweza kutoa gawio kwa TANESCO kwa sababu kampuni ikifanya vizuri inaweza kutoa gawio kwa shirika" alimaliza Maharage.

Nae Mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya uzalishaji wa nguzo za zege (TCPM) Jema Msuya ameishukuru bodi ya Shirika kwa kuwaamini na kuwateua kuongoza bodi hiyo.

"Tunaushukuru uongozi wa bodi ya TANESCO pamoja na mkurugenzi kwa kutuamini na na kutupa nafasi ya kuongoza bodi mpya ya TCPM na tutahakikisha upatikanaji na uzalishaji unaotakiwa wa nguzo bora ambazo TANESCO watazitumia katika kuongeza na kusambaza umeme" amesema Msuya

Naye Prof.Shubi Kaijage, ambaye ni mwenyekiti wa kampuni ya uendelezaji joto ardhi Tanzania (TGDC) ameeleza masuala mbalimbali ya utekelezaji ambayo atayafanyia kazi katika majukumu yake.

"Tuna maeneo manne tutakayojikita zaidi ni katika masuala ya uendelezaji wa utafiti katika maeneo ya jotoardhi sababu teknolojia hii ni mpya katika maeneo yetu ya Tanzania, kuongeza na kupata vitendea kazi vilivyo bora pamoja na uwezo wa wafanyakazi,kuongeza idadi ya wafanyakazi na kuhakikisha kampuni inajiendesha kwa tija" amesema.

Kuundwa kwa bodi hizo mbili kunalenga kuongeza ufanisi na utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Shirika pamoja na kampuni zake tanzu ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya umeme unakua wa uhakika na kwa gharama nafuu.