Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania

Tanzania Geothermal Development Company

(TGDC)

Kampuni ya TGDC yafanya Semina kwa Wabunge wa Kamati ya Nishati na Madini jijini Dodoma. Imewekwa: 21st June, 2017

Imeelezwa kuwa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) itazalisha Megawati 200-600 kutokana na Jotoardhi ifikapo 2025.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani katika Semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Dkt. Kalemani ameielezea Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini kuwa TGDC ina jukumu la kuendeleza nishati ya Jotoardhi kwa niaba ya Serikali ya Tanzania ili kukuza uchumi na kuongeza ajira.

Aliongeza kuwa, Tanzania ina reserve ya Jotoardhi inayokadiliwa kuzidi Megawati 5000 na inapatikana maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Mbeya, Songwe, Rukwa, Dodoma, Singida, Shinyanga, Morogoro, Pwani, Mara, Kagera na Arusha.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Kato Kabaka ameieleza Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuwa, Kampuni ya TGDC ina majukumu mengi likiwemo jukumu la kuendelea kuhimiza matumizi mengine ya nishati ya Jotoardhi (direct heat use).

Aliongeza kuwa TGDC itaanza kuzalisha megawati 30 ifikapo 2018 kutoka Mradi wa Ngozi ambapo utafiti umefanyika kwa kiasi kikubwa.

Mhandisi Kabaka ameelezea upatikanaji wa jotoardhi ambao unatokana na mchakato wa kinyukilia ndani ya tufe la dunia, ambalo ni endelevu na mchakato huu hutokea kwenye nyufa zilizopo kwenye gamba la dunia.

Aidha, ameeleza kuwa tofauti na upatikanaji wa nishati ya umeme, jotoardhi inajumuisha vitu vingi ikiwa ni pamoja na gesi ya Carbon oxide, sulphur na madini mbalimbali ambayo hutumika viwandani na manyumbani.

“Jotoardhi hutumika katika ukaushaji mazao ya kilimo, uzalishaji wa mbogamboga, ufugaji wa samaki, utalii wa kibiashara, mabwawa ya kuogelea na usambazaji wa Joto kwenye Nyuma,” Alisema Mhadisi Kabaka.

Pia, Mhandisi Kabaka alisema kuwa uzalishaji wa Jotoardhi ni rafiki kwa mazingira ukilinganisha na vyanzo vingine vya nishati ya umeme.

Mara baada ya Semina hiyo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Mbuge wa Ludewa, Deo Ngalawa amesema kuwa anaishukuru Wizara ya Nishati na Madini kupitia Kampuni ya TGDC kwa kuwajengea uwezo katika nishati ya Jotoardhi na kufahamu faida za nishati hiyo nchini.

Aliongeza kuwa ipo haja ya Kampuni ya TGDC kuwa na Sheria ambayo itasaidia katika Uendelezaji wa Jotoardhi na kuagiza Wizara, sasa kuhakikisha kuwa TGDC hailipia leseni ya utafiti ili kufanikisha zoezi la upatikanaji wa nishati hiyo.

Jotoardhi inazalishwa katika nchi zaidi ya 26 duniani na zaidi ya Gigawati 12.6 zilipatika mwaka 2015, na zaidi ya nchi 90 zina maeneo yenye rasilimali ya jotoardhi.